Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
United Nations
Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Location:
New Rochelle, NY
Genres:
News & Politics Podcasts
Networks:
United Nations
Description:
Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Twitter:
@HabarizaUN
Language:
Swahili
Contact:
9178215291
Episodes
Jinsi usawa wa kijinsia na rika katika umiliki wa ardhi unavyochochea ukulima na uhakika wa chakula Kenya
11/21/2024
Mpango wa Usimamizi wa Ardhi (Land Governance program) uliopatiwa jina "Kusaidia kufikia Ajenda 2030 kupitia mageuzi chanya ya ugatuzi wa ardhi (land reforms) katika maeneo ya ardhi za jamii nchini Kenya" umeboresha uhakika wa kupatikana kwa chakula na lishe kupitia upatikanaji wa ardhi kwa wote nchini Kenya. Programu hii imezinduliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kilimo na chakula FAO kwa kushirikiana na Muungano wa Ulaya (EU) katika kaunti 9 ikilenga kuimarisha sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi na umeimarisha usimamizi wa ardhi kwa ajili ya maisha bora na maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika kaunti zote zinazotekeleza. Kupitia video iliyoandaliwa na FAO, Cecily Kariuki anaeleza matokeo yake.
Duration:00:05:05
21 NOVEMBA 2024
11/21/2024
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka nchini Kenya kushuhudia jinsi mpango wa Usimamizi wa Ardhi uliopatiwa wa "kusaidia jamii kufikia Ajenda 2030” ambao FAO imetekeleza kwa kaunti kadhaa. Pia tunakuletea muhtasari wa habari na uchambuzi wa neno.Hague kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ICC ambayo leo imetoa kibali cha kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, Waziri wa zamani wa ulinzi Yoav Galant na kiongozi wa kundi la kipalestina la Hamas Mohamed Diab Ibrahim al-Masri alimaarufu kama kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhaifu wa vita ulitendeka wakati wa vita inayoendelea baina ya Israel na Hamas.Mjini Baku nchini Azerbaijan mkutano wa 29 wa mkataba wa nchi wanachanama wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabainchi COP29 unaelekea ukingoni na leo ukijikita na masuala ya kijinsia na mabadiliko ya tabianchi. Miongoni mwa waliozungumzia changamoto ya tabianchi kwa wanawake ni Jemimah Njuki, mkuu wa kitengo cha uwezeshaji wa kiuchumi katika shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake UN Women.“Raia wanaoshtakiwa katika mahakama za kijeshi nchini Uganda hukosa dhamana sawa ya mchakato wa kisheria kama wale wanaoshtakiwa katika mahakama za kiraia,” amesema Volker Türk, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu hii leo kufuatia tukio la kutekwa kwa mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Kiiza Besigye akiwa nchini Kenya.Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili na hii leo Dkt. Mwanahija Ali Juma, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili, Zanzibar nchini Tanzania, BAKIZA anafafanua maana ya neno MHARABU”.Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!
Duration:00:09:59
COP29 Georgina Magesa: Watoto wana haki ya kuishi katika mazingira salama
11/20/2024
Mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP29 unaoendelea huko Baku Azerbaijan umeleta pia watoto na vijana wanaharakati wa mazingiria kutoka kote ulimwenguni na kuwapatia fursa kuketi katika meza moja na viongozi ili kuhakikisha mustakabali wao umewekwa katika ajenda ya mkataba huo. Jukumu lao kama wachechemuzi wa mabadiliko chanya na hitaji la mazungumzo na ushirikiano kati ya vizazi lilitambuliwa rasmi katika matokeo ya Mkutano wa Zama Zijazo, SOTF mnamo Septemba 2024.Georgina Magesa, msichana mwenye umri wa miaka tisa na mwanaharakati wa mazingira, ambaye amewakilisha watoto wenzake kutoka Tanzania katika Mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP29 huko Baku, Azerbaijan. Anatoa ujumbe mahsusi akianza kwa kusistiza kuwa watoto pia wana mchango katika kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi.“Watoto wenzangu duniani kote, nyie pia mnaweza kuleta mabadiliko chanya. Anza na hatua ndogo pia muwe na ndoto kubwa. Panda miti. Hifadhi maji. Jifunze kuhusu mazingira yetu. Kwa Pamoja vitendo vyetu vidogo vitageuka mabadiliko makubwa”Katika mwaka huu wa 2024 ambao viwango vya joto duniani vimevunja rekodi duniani, watoto na vijana wanaendelea kupaza sauti zao wakihimiza viongozi wa dunia kuchukua hatua za haraka zinazohitajika ili kushughulikia janga la mabadiliko ya tabianchi. Georgina anasema Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF liko mstari wa mbele, lakini sasa ni wakati wa mshikamano kwa ajili ya mazingira bora kwa watoto wa leo, na wa zama zijazo..“Kwa viongozi wa dunia walioko hapa leo, hii si kazi ya UNICEF pekee. UNICEF inafanya kazi nzuri na sisi watoto, lakini tunahitaji msaada wako ili kujenga ulimwengu wa kesho ambapo hakuna mtoto anayepaswa kuchagua kati ya afya na elimu yake; ambapo hakuna mtoto anayekunywa maji yasiyo salama; hakuna mtoto anayekosa shule kwa sababu ya masuala yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi; na ambapo kila mtoto ana nafasi ya kuwa na afya bora na elimu bora.”Georgina anatamatisha kwa kusisitiza kuwa janga la mabadiliko ya tabianchi limenyima watoto haki zao hivyo kwa kila mtu...“Kumbuka unapolinda mazingira unalinda afya, elimu na ndoto za watoto. Mtoto mwenye afya bora na elimu bora anaweza kubadilisha ulimwengu.”Ama kweli watoto wana haki ya kuishi katika mazingira salama!
Duration:00:04:01
20 NOVEMBA 2024
11/20/2024
Hii leo jaridani tunaangazia ripoti siku ya watoto duniani, na kwa kutambua siku hii tunamulika mikutano yote yanayoendelea kwa ajili ya haki za watoto na vijana, ambao wametoa ujumbe wao kutoka Baku nchini Azerbaijan na Denmark wakiwakilisha nchi zao.Leo ni siku ya watoto duniani maudhui mwaka huu yakiwa "Kila mtoto, kila haki"na katika kuhakikisha sauti zao zinasikika kuhusu mustakbali wa utakao, shirika la Umoja wa Maataifa la kuhudumia watoto duniani UNICEF limewapa fursa ya kuandika barua kwenda kwa watu wazima kote duniani ili kutoa madukuduku yao na kutanabaisha wanachokitaka kwa ajili ya mustakbali wao.Kama ulivyosikia katika taarifa yetu ya kwanza leo ni siku ya watoto duniani ikirejelea tarehe 20 Novemba mwaka 1954 kwa mara ya kwanza kabisa ilipoanzishwa na Umoja wa Mataifa kusongesha umoja na kujitambua miongoni mwa watoto duniani..Makala ikiwa leo ni siku ya watoto duniani, tunakupeleka Baku Azerbaijan katika mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP29, ambako Selina Jerobon amefuatilia mkutano wa watoto na vijana inayomulika mchango wao katika kuhakikisha mazingira bora.Mashinani katika kuadhimisha siku ya watoto duniani tunabisha hodi msitu wa Amazoni nchini Peru kwa mtoto Susan akitoa wito kwa dunia kuchukua hatua dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kulinda msitu huo kunusuru kizazi cha watoto wa sasa na wa vizazi vijavyo katika taifa hilo.Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!
Duration:00:09:57
UNICEF - Maadhimisho ya kimataifa ya siku ya mtoto duniani yafanyika Denmark
11/20/2024
Leo ikiwa ni siku ya watoto duniani ikirejelea tarehe 20 Novemba mwaka 1954 kwa mara ya kwanza kabisa ilipoanzishwa na Umoja wa Mataifa ili kusongesha umoja na kujitambua miongoni mwa watoto duniani. Kisha siku hii ikaongezwa nguvu na Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto duniani mwaka 1959 na hatimaye mwaka 1989 Baraza hilo lililopitisha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto, CRC. Mkataba unatambua haki kuu nne za msingi za mtoto: Kuishi, Kuendelezwa, Kulindwa na Kushirikishwa. Hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limefanya maadhimisho ya kimataifa huko Copenhagen Denmark, na Madina Jubilate, Mchechemu wa UNICEF Tanzania kwa Tabianchi anaelezea alivyoshiriki.
Duration:00:01:50
Waraka kutoka kwa watoto: Kwenu watu wazima, kwa nini mnauruhusu mustakbali wetu kuwekwa rehani?
11/20/2024
Leo ni siku ya watoto duniani maudhui mwaka huu yakiwa "Kila mtoto, kila haki"na katika kuhakikisha sauti zao zinasikika kuhusu mustakbali wa utakao, shirika la Umoja wa Maataifa la kuhudumia watoto duniani UNICEF limewapa fursa ya kuandika barua kwenda kwa watu wazima kote duniani ili kutoa madukuduku yao na kutanabaisha wanachokitaka kwa ajili ya mustakbali wao. Hao ni baadhi tu ya makumi ya watoto walioandika barua , hawa ni kutoka Gaza, Tanzania na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC ambao walishika kalamu na karatasi kufikisha ujumbe wao kwa watu wazima wa dunia ya sasa iliyoghubikwa na changamoto lukuki zinazoweka rehani mustakbali wao.Kwa mujibu wa ripoti mpya ya UNICEF ya “Hali ya watoto duniani mwaka 2024: Mustakabali wa Utoto katika Ulimwengu Unaobadilika,” iliyotolewa leo sanjari na maadhimisho ya siku hii kuna masuala matatu makubwa ya kimataifa yatakatoathiri maisha ya watoto ifikapo 2050 na kuendelea. Mosi ni mabadiliko katika idadi ya watu, pili janga la mabadiliko ya tabianchi na migogoro na tatu teknolojiaUNICEF inasema yote haya ni changamoto na fursa ambazo watoto wanaweza kukabiliana nazo katika zama zijazo.Rafif mtoto mkimbizi wa ndani ameandika barua kutoka Palestina ambako vita imetamalaki, anasema“Ninatoka mjini Gaza na sasa nimefurushwa hadi Kusini mwa Gaza. kama watoto Ni haki yetu kuishi kwa usalama na kujenga mustakbali bora”Kutoka mashariki ya Kati hadi Afrika Mashariki kwa Steven akimulika afya“Na nianaandika kwenu kutoka Tanzania. Kwenye jamii yangu watoto wanaugua kila wakati , kwa nini? Huu ndio mustakbali wangu je unasikiliza?”Nako Congo DRC mitihani ni mingi, Andrea anasema“Nataka kushuhudia dunia ambayo kila mtoto anapendwa, dunia ambayo amani inashamiri ni raha na faraja. Napenda kuona hasira zinageuka na kuwa mazungumzo”Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiunga mkono suti hizo za watoto katika ujumbe wake amesema Katika Siku ya Watoto Duniani tunasherehekea washiriki wachanga zaidi wa familia yetu ya kibinadamu. Lakini leo pia ni wakati wa kutambua changamoto kubwa zinazowakabili watoto katika ulimwengu wetu uliogawanyika sana, wenye misukosuko na mara nyingi ulioshamiri ukatili.”Ripoti ya UNICEF imetoa wito wa kuwekeza katika elimu, miji endelevu na yenye mnepo kwa watoto, miundombinu inayohimili mabadiliko ya tabianchi, teknolojia, huduma muhimu na mifumo ya msaada wa kijamii na pia teknolojia iliyo salama kwa watoto ili kupambana na mzigo wa changamoto zinazowakabili.
Duration:00:02:20
19 NOVEMBA 2024
11/19/2024
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka Baku nchini Azerbaijan kwenye mkutano wa COP29. Miongoni mwa mambo yanayopigiwa chepuo ni madini ya kimkakati yanayoelezwa kuwa ni jawabu la nishati chafuzi kwa mazingira na tunapata ufafanuzi kutoka kwa Adam Anthony, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiRasilimali nchini Tanzania.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amewasihi viongozi wa kundi la nchi 20 zenye uchumi mkubwa zaidi duniani, G20 wanaokutana huko Rio De Janeiro, Brazil kuwaagiza mawaziri na washawishi wao huko COP29 wahakikishe wanakubaliana juu ya lengo jipya na kubwa la mwaka huu la ufadhili kwa tabianchi nchi. Guterres amesema sambamba na hilo ni vema kukabiliana na taarifa potofu kuhusu tabianchi.Huko Kusini mwa Lebanon, walinda amani wanaohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kikosi cha Mpito nchini humo, UNIFIL, wameshuhudia uharibifu mkubwa wa kutisha kwenye vijiji vilivyoko sambamba na eneo la kati ya Israeli na Lebanon lisilopaswa kuwa na mapigano, huku hali ya watoto nchini humo ikizidi kuwa mbaya.Hii leo ni siku ya choo duniani ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema licha ya choo kuwa ni msingi wa kusongesha afya ya binadamu na kusaidia watoto wa kike na wanawake kuishi maisha ya utu, bado wakazi wengi wa dunia hususan kwenye mizozo na majanga wanaishi bila huduma hiyo ya msingi.Mashinani tunasalia huko huko Baku, kwenye COP29 ambapo nampisha msichana mwanaharakati wa mazingira kutoka Tanzania, akieleza ni nini anafanya na nini atakachoondoka nacho kwenye mkutano huo.Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!
Duration:00:11:07
Uganda inaendelea na mapambano ya kutunza wakimbizi licha ya changamoto za kifedha
11/18/2024
Kwa miongo kadhaa sasa mfumo wa Uganda wa kuwaweka wakimbizi kwenye makazi badala ya kambi, umesaidia kujengea mnepo wakimbizi na hivyo wanaweza kujitegemea. Wakimbizi wanapata huduma za msingi kama vile hata ardhi ya kulima na kufugia mifugo ili kujipatia kipato. Kupitia video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Selina Jerobon amefuatilia hadithi ya mama mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambaye baada ya kupitia machungu na kukimbilia nchini Uganda sasa ameanza kuwa na matumaini ingawa ukata unatishia huduma kama alivyojionea mwenyewe Fillipo Grandi, Kamishna Mkuu wa shirika hilo.
Duration:00:05:11
Vijana wafurahia stadi za kuondokana na umaskini Sudan Kusini
11/18/2024
Vijana katika mji wa Tambura ulioko jimbo la Equatoria Magharibi nchini Sudan Kusini wanageuza mafunzo ya ufundi stadi kuwa nguvu ya amani na ustawi, mafunzo ambayo yalifanikishwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, UNMISS.Shamrashamra zilitawala wakati vijana 61, wakiwemo wasichana 41 na wavulana 20 walipohitimu mafunzo ya ufundi stadi yenye lengo la kuwaondoa katika umaskini na pia kuwaepusha kutumikishwa katika mzozo unaoendelea nchini humo tangu Desemba 2013.Walifundishwa urembo wa nywele, kutengeneza sabuni, halikadhalika ushoni, mafunzo yaliyofadhiliwa na UNMISS na kutolewa na shirika la kiraia Star Trust Organization, linalohusika na kupunguza ghasia kwenye jamii kwa kuwajegena vijana uwezo.Miongoni mwao ni Suzan James, mama wa watoto wawili aliyejifunza urembo wa nywele na akiwa anamhudumia mteja wakati wa mafunzo anasema.“Ninashukuru mno, kwa sababu nimejifunza mambo mengi ambayo awali sikuyafahamu, lakini sasa ninaweza kufanya. Inanisaidia sana, na ninajivunia na nina furaha. Baada ya hili, nitaenda kufungua sehemu yangu mwenyewe ya urembo wa nywele ili kusaidia jamii.”Huyu ni Justin Alex yeye amejifunza ushoni na akiwa kwenye chereheni yake anasema.. “iwapo nitapekela hii cherehani nyumbani, nitaweza kufanya kazi na kusaidia familia yangu. Kama kijana tusikae nyumbani au tusifanye uhalifu mjini na kusababisha vifo kwa jamii zetu kwa sababu si jambo zuri. Kuanzia sasa tunahitajika kushiriki kwenye shughuli za kusaidia jamii, kama kupeleka hii cherehani nyumbani ili nisaidie jamii yangu.”Wahitimu wamepatiwa vifaa vya kuanzia kufanyie kile walichojifunza. Katika hafla ya utoaji wa vyeti UNMISS iliwakilishwa na afisa wake wa masuala ya ulinzi na ujumuishaji kwenye jamii Ibrahim Tahiru ambaye amesema..“Mradi huu unaweza kuleta amani, lakini pia mradi huu huu unahitaji amani ili uweze kuendelea. Bila amani hivi vitu vitakuwa bure. Kwa sababu wahitimu wanahitaji mazingira yenye amani ili waweze kutumia stadi zao kwa ajili ya kuboresha maisha yao na ya jamii zao. Mradi huu ni ishara ya nia yetu ya kuendelea kushirikiana na Sudan Kusini na kusaidia kufikia amani ya kudumu na kuondokana na umaskini.”Mamlaka za Tambura zina Imani kubwa na mradi huu kama asemavyo Kaimu Kamishna wa Tambura Moses Masisere.“Hakika, Tambura tumekuwa tukililia amani. Kwa hiyo kwa msaada huu tunaamini kuwa mafunzo kwa vijana zaidi kutawasaidia washiriki kwenye harakati za kiuchumi na kupunguza mauaji na uhalifu mwingine Tambura.”
Duration:00:01:57
18 NOVEMBA 2024
11/18/2024
Hii leo jaridani tunaangazia wakimbizi wa ndani nchini Haiti, na mafunzo ya stadi za kujikimu kimaishwa kwa vijana Tambura Sudan Kusini. Makala inatupeleka nchini Uganda na mashinani nchini Kenya, kulikoni?Zaidi ya watu 20,000 wamekimbia makazi yao katika mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince katika muda wa siku nne tu, ikiwa ni pamoja na watu wengine zaidi ya 17,000 wanaohifadhiwa katika makazi 15 ya wakimbizi wa ndani, kutokana na kuongezeka kwa ghasia za magenge ya uhalifu ambazo ziumevuruga kabisa minyororo muhimu ya usambazaji wa misaada na kulitenga jiji la Port-au-Prince (POTOPRINSI) limesema shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM.Vijana katika mji wa Tambura ulioko jimbo la Equatoria Magharibi nchini Sudan Kusini wanageuza mafunzo ya ufundi stadi kuwa nguvu ya amani na ustawi, mafunzo ambayo yalifanikishwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, UNMISS.Katika makala Selina Jerobon kupitia video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi anakupeleka Uganda kuona harakati za wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kujikwamua kiuchumi baada ya machungu waliyopitia nyumbani kwao.Mashinani tutaelekea nchini Kenya kusikia ni kwa jinsi gani jamii katika maeneo kame wanakabiliana na mabadiliko ya tabianchi.Mwenyeji wako ni Bosco Cosma, karibu!
Duration:00:10:46
IOM: Zaidi ya watu 20,000 wamefuriushwa ndani ya siku 4 Haiti kutokana na machafuko ya magenge ya uhalifu
11/18/2024
Zaidi ya watu 20,000 wamekimbia makazi yao katika mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince katika muda wa siku nne tu, ikiwa ni pamoja na watu wengine zaidi ya 17,000 wanaohifadhiwa katika makazi 15 ya wakimbizi wa ndani, kutokana na kuongezeka kwa ghasia za magenge ya uhalifu ambazo ziumevuruga kabisa minyororo muhimu ya usambazaji wa misaada na kulitenga jiji la Port-au-Prince (POTOPRINSI) limesema shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM. Kupitia taarifa iliyotolewa leo na IOM nmini Port-au-Prince asilimia kubwa ya watu hawa waliofurushwa makwao wametawanywa zaidi ya mara moja wakilazimika kukimbia na kuacha kila kitu walichokuwa nacho na shirikika hilo linasema kiwango hiki cha watu kutawanywa hakijashuhudiwa Haiti tangu Agost 2023.Shirika hilo linasema kufungwa kwa usafiri wa anga kufuatia shambulizi lililolenga ndege tatu za kibiashara mjini Port-au-Prince, kuzuia ufikiaji wa bandari kuu ya nchi hiyo, na barabara zisizo salama zinazodhibitiwa na makundi yenye silaha kumeliacha eneo la Katikati ya mji mkuu taabani na kutengwa bila msaada na hivyo kuzidisha mateso kwa watu ambao tayari wako hatarini.Mkuu wa IOM nchini Haiti Grégoire Goodstein ameonya kwamba "Kutengwa kwa Port-au-Prince kunaongeza janga la ibinadamu. Uwezo wetu wa kutoa misaada umewekwa njiapanda na bila msaada wa haraka wa kimataifa, mateso yataongezeka sana kwa raia wa Haiti huku kukiwa na asilimia 20 pekee ya mji wa Port-au-Prince inayofikika, wakati wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wanakabiliwa na changamoto kubwa katika kufikia watu walioathirika.”Kulingana na Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR, vikundi vya uhalifu katika mji mkuu wa Hati vinaendelea kupanuka wigo vikichukua udhibiti wa vitongoji vya ziada na kutenganisha zaidi jamii.Hadi sasa ofisi hiyo inasema ghasia zinazohusiana na magenge zimesababisha karibu vifo 4,000 mwaka 2024, unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kingono unaotumiwa kama silaha ya ugaidi, umefikia viwango vya kutisha.Pia imesema wanawake na watoto wameathiriwa kupita kiasi, huku asilimia 94 ya wanawake na wasichana waliokimbia makazi yao wakiwa katika hatari kubwa ya kudhulumiwa kingono.Licha ya changamoto hizi, IOM na washirika wake wameahidi kuendelea kutoa msaada wa kuokoa maisha.IOM pia inatoa wito wa kuongeza haraka ufadhili kwa shughuli za kibinadamu Haiti kwani hadi kufikia mwezi huu wa Novemba, ombi la dola milioni 674 la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Haiti limefadhiliwa kwa asilimia 42 pekee, na kuwaacha mamilioni ya watu bila msaada wanaohitaji.
Duration:00:02:06
Esneda kutoka jamii ya Yukpa asema haogopi vitisho kutetea eneo la jamii yao ya asili nchini Colombia
11/15/2024
Jamii ya asili ya Yukpa nchini Colombia imevumilia miongo kadhaa ya migogoro na watu kutawanywa inayosababishwa sio tu na mabadiliko ya tabianchi mila kandamizi bali pia kupotea kwa viumbe hai na hivyo kutishia maisha yao. Esneda Saveedra, Kiongozi wa jamii ya asili ya Yukpa nchini Colombia akiwa anazungumza akiketi ndani ya msitu na kando ya mto Maracas., anasema hana hofu ya kutetea ardhi hii.Ardhi anayozungumzia ni eneo hilo la mto Maracas anayotetea dhidi ya vitisho kutoka kwa waharibifu wa mazingira kufuatia yale yaliyojadiliwa katika mkutano wa 16 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa bayonuai, COP16 uliomalizika Ijumaa iliyopita huko mjini Cali nchini Colombia."Sina hofu ya kutetea ardhi hii. Yale niliyopitia kama mtoto, changamoto zote hizo, yalinipa nguvu, yalinipa ujasiri, na yakaondoa hofu yangu."Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR inatupatia taswira ya juu ya eneo la makazi ya jamii ya Yukpa, msitu mnene na kisha kwenye mto Maracas, shughuli zinaendelea, wengine wakiogelea, wengine wakivua samaki, mama mmoja akisafisha kuku aliyemaliza kumchuna.Esneda anaeleza umuhimu wa mto huu kwa maisha ya jamii yake na anaendelea kujitahidi ili kulinda mazingira hayo."Huu ni mto Maracas, ambapo watu wetu, mababu zangu, walivua samaki kwa ajili ya chakula kila siku. Waliharibu mazingira kwa kukata miti yote, na matokeo yake, mto ulianza kukauka. Leo, mto Maracas hauna mtiririko wa maji kama ulivyokuwa zaidi ya miaka 20 iliyopita."Katika juhudi zake, Esneda ameanzisha mazungumzo na maafisa wa serikali katika manispaa ya Becerril, akijaribu kuleta mabadiliko na uelewa juu ya umuhimu wa kuhifadhi ardhi na utamaduni wa watu wa Yukpa."Kumekuwa na uratibu, kazi ya pamoja, na jambo muhimu zaidi kwangu kama mwanamke wa Yukpa imekuwa kuleta ufahamu kuhusu watu wa Yukpa na ardhi yetu. Mabadiliko ya tabianchi yametufikisha kwenye tatizo kubwa zaidi, ambalo ni upotevu wa mazao na ukosefu wa chakula. Leo hatuna chakula cha kutosha katika jamii zetu. Tunaendelea kupambana, lakini pia tuko hapa kusaidia dunia nzima kuendelea kupambana na kulinda mazingira, ardhi, na hewa. Na kusema: 'Tupo hapa kuchangia kwa ajili ya ubinadamu, kwa ulimwengu mzima.’"Harakati zake zimekumbwa na vitisho.“Walinitishia hapa kwa kuzungumza, na kwa kusema ukweli. Mama yangu alikuwa kiongozi thabiti—na bado ni kiongozi thabiti. Na nilipokuwa mdogo, nilimsindikiza kwenye michakato yake yote ya harakati, mipango na uongozi. Niliendeleza njia hiyo ya uongozi kwa sababu niliona ni muhimu. Ilikuwa ni wajibu wangu. Nilijiambia, ‘mimi ni mwanamke ambaye nimezaliwa kutetea eneo hili.”Kwa Esneda, kulinda ardhi ya Yukpa ni zaidi ya wajibu; ni dhamira ya kuhifadhi urithi wa mababu zake. Katika changamoto za kila siku, Esneda anabaki imara kwa matumaini kuwa jamii yake na mchango wao katika kuhifadhi mazingira utatambuliwa ulimwenguni.
Duration:00:03:39
Anne Tek: COP29 isiwape kisogo wanawake wanaokabiliiwa na athari za mabadiliko ya tabianchi Afrika
11/15/2024
Mkutano wa 29 wa Umoja wa Mataifa wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi COP29 ukianza wiki ya piili mjini Baku Azerbaijan leo, wito umetolewa kwa wanawake amba oni waathirika wakubwa wa janga la mabadiliko ya tabianchi kutopewa kisogo. Anne Cheruto Tek ambaye amebeba bendera ya wanawake waathitika wa mabadiliko ya tabianchi kutoka Afrika ameiambia UN News anachokifanya COP29..“Sana sana kufuatilia haya madhara ya mabadiliko ya tabianchi hasa kwa wanawake na vijana barani Afrika. Sana sana utakuwa wanawake ndio wanaoshughulikia masuala ya maji, masuala ya kuni, masuala ya chakula , lakini mara nyingi kukiwa na janga la mabadiliko ya tabianchi kama ukame, mafuriko, wanawake ndio wanaangamia zaidi, kwa sababu wanawke ndio wanakuwa na jukumu la kuendesha nyumba na hivyo hawana nafasi ya kutafuta fedhha ambaz zinaweza kuwasaidia wakati wa majanga hayo.”Na kutokana na hayo anasema wanawake hukabiliwa na changamoto kubwa“Wengi hupata magonjwa , wengi huathhirika sana wakati wa majanga ikiwemo vifo, ukosefu wa fedha na pia ukatili wa kijinsia wakati wa shida za mabadiliko ya tabianchi.”Na nini ombi lake katika mkutano huo?Kuhakikisha kuwa hizi changamoto zinaangaziwa hasa kwa masuala ya fedha, kuhakikisha kuwa fedha zinawafikia wanawake vijijini , kuhakikisha kuwa wanaweza kuelewa masuala ya mabadiliko ya tabianchi na pia waweze kuelezea hadithi zao jinsi wanavyoathirika na tunaomba hii COP kuangazia haya majanga hasa kwa wanawake, wasichana na watu wasiojiweza kama wenye ulemavu.”
Duration:00:01:52
15 NOVEMBA 2024
11/15/2024
Hii leo jaridani tunaangazia suala muhimu wa mabadiliko ya tabianchi tukijikita kataika mkutano wa COP29 huko Baku Azerbaijan kuwasikia wanaharakati wa mazingira kutoka nchi mbalimbali.Mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP29 u unaofanyika Baku Azerbaijan, leo umejikita na ongezeko la gesi chafuzi ya methane ambayo kwa kiasi kikubwa inatokana na shughuli za binadamu ikiwemo ufugaji wa ng’ombe, na sasa nini kifanyike ili kuidhibiti.Tunasalia huko huko Baku, Azerbaijan. Wito umetolewa kwa wanawake ambao ni waathirika wakubwa wa janga la mabadiliko ya tabianchi wasipewe kisogo katika harakati za kuhimili na kukabili madhara ya janga hilo.Katika makala Bosco Cosmas anatupeleka Amerika ya Kusini kusikia harakati za mwanamke wa jamii ya asili za kulinda eneo lao.Mashinani leo Fathimath, kijana kutoka Maldives anatoa kauli kwa ajili ya hatua za dharura kupambana na mabadiliko ya tabianchi katika mkutano wa COP29.Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!
Duration:00:09:58
UNEP: Licha ya taarifa za ongezeko la gesi ya methane hatua zinazochukuliwa ni kidogo
11/15/2024
Mkutano wa 29 wa mkataba wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi COP29 unaofanyika Baku Aberbaijana leo umejikita na ongezeko la gesi ya methane ambayo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na shughuli za binadamu na nini kifanyike kuidhibiti. FKulingana na ripoti iliyozinduliwa leo na shirika la Umoja wa Mataifa wa mazingira UNEP katika mkutano huo, mfumo wa teknolojia ya hali ya juu ambao unatambua uvujaji mkubwa wa gesi ya methane umewasilisha tarifa 1,200 kwa serikali na makampuni katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, lakini ni asilimia moja tu ya taarifa hizo ndizo zilizofanyiwa kazi.Ripoti hiyo mpya iliyopewa jina “Jicho kwenye methane: Haionekani lakini inashuhudiwa” inasema licha ya ahadi zilizotolewa chini ya makubaliano ya ahadi za kimataifa za kupunguza uzalishaji wa gesi ya methane kwa asilimia 30 ifikapo 2030 hatua zinazochukuliwa hazitoshelezi kupunguza gesi hiyo.Ripoti imeangazia tahadhari za methane kutoka kwenye Mfumo wa Tahadhari na hatua dhidi ya Methane MARS, ambayo ni sehemu ya UNEP ya uangalizi wa kimataifa wa uzalishaji wa methane IMEO ambayo unawakilisha fursa ambazo haijatumiwa kwa hatua za haraka dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.Akizindua ripoti hiyo Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, amesema ili kuwa na nafasi yoyote ya kudhibiti ongezeko la joto duniani, uzalishaji wa methane lazima ushuke, na ushuke haraka."Tunapozingatia kuwa ni asilimia 1 tu ya taarifa 1200 ambazo tulitoa ndizo zilisababisha hatua kuchukuliwa, basi hauitaji kuwa mtaalamu wa hesabu ili kuhesabu ushindi mkubwa unaowezekana hapa. Tuna mifumo iliyothibitishwa ya kutambua uvujaji Mkubwa wa gesi ya methane ili uweze kukomeshwa haraka, mara nyingi kwa ukarabati rahisi na wakati mwingine tunazungumza juu ya kukaza mipira au kubadilisha vichungi.”Ameongeza, kuwa "Serikali na makampuni ya mafuta na gesi ambayo sehemu kubwa ya uchumi wa dunia bado inawategemea lazima waache kupiga domo kwa changamoto hii wakati majawabu yanawatazama usoni. Badala yake, wanapaswa kutambua fursa muhimu ambayo mfumo huu unatoa na kuanza kuchukua hatua kutokana na taarifa kwa kuziba uvujaji ambao unamwaga gesi ya methane ya joto kwenye angahewa.”Amehitimisha kwa kusema, "Serikali na sekta binafsi lazima zizuie uzalishaji wa methane, na lazima zifanye hivyo sasa."Gesi ya Methane kwenye angahewa ni kichocheo cha pili kikubwa cha ongezeko la joto duniani baada ya hewa ya ukaa au CO2 na ina nguvu zaidi ya mara 80 kuliko hewa ya ukaa katika kusambaa kwa muda mfupi.UNEP imesisitiza kuwa utoaji wa gesi ya methane duniani lazima upunguzwe kwa asilimia 40 hadi 45 ifikapo 2030 ili kufikia njia za gharama nafuu zinazopunguza ongezeko la joto duniani hadi kufikia nyuzi joto 1.5°C.Bado taarifa za sayansi za hivi karibuni zinaonyesha viwango vya angahewa vya methane vimepanda kwa kasi iliyovunja rekodi katika kipindi cha miaka 5 iliyopita.
Duration:00:02:05
Jifunze Kiswahili - Ufafanuzi wa maneno “MADHALI, WAMA, FALAU NA HOBE”
11/14/2024
Katika kujifunza lugha ya Kiswahili hii leo mchambuzi wetu mlumbi wa Kiswahili Joramu Nkumbi kutoka nchini Tanzania, anafafanua maana ya maneno “MADHALI, WAMA, FALAU NA HOBE”
Duration:00:01:05
14 NOVEMBA 2024
11/14/2024
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka Baku kwa mkutan wa COP29, amabyo washiriki wanasaka mbinu za kujumuisha makundi yote katika harakati za kukabili na kuhimili madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanayochochewa na ongezeko la hewa chafuzi. Idhaa ya Kiswahili imezungumza na Naomi mmjoja wao kutoka Tanzania. Pata pia muhtasari wa habari na ujifunze Kiswahili.Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kuelimisha umma kuhusu ugonjwa wa kisukari, shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO leo limesema idadi ya watu wazima wanaoishi na Kkisukari duniani ni zaidi ya milioni 8000 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya mara 4 tangu mwaka 1990.Baku Azerbaijan ambako mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP29 leo umejikita na na lengo la kutozalisha kabisa hewa ya ukaa ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antinio Guterres ameainisha jukumu muhimu ambalo miji, mikoa, biashara na taasisi za kifedha lazima zitekeleze katika kuendesha juhudi za dunia nzima kufikia lengo la kutozalisha kabisa hewa ya ukaa katikati ya karne hii.Nchini Sudan shirika la Umojja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharida OCHA limesema ghasia za kutumia silaha na mashambulizi katika Jimbo la Aj Jazirah zinadhihirisha ukatili wa karibu miezi 19 ya vita nchini Sudan,huku kukiwa na ripoti za ubakaji, mauaji ya halaiki na uporaji mkubwa. Katika chini ya wiki mbili, OCHA inasema uhasama huko Aj Jazirah umefurusha zaidi ya watu 135,000 kutoka makwao, wengi wao walikimbilia majimbo jirani ya Gedaref na Kassala.Katika kujifunza lugha ya Kiswahili hii leo mchambuzi wetu mlumbi wa Kiswahili Joramu Nkumbi kutoka nchini Tanzania, anafafanua maana ya maneno “MADHALI, WAMA, FALAU NA HOBE”Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!
Duration:00:09:59
Wananchi tufahamishwe kwa kina majukumu ya MONUSCO ili kukabili habari potofu DRC
11/13/2024
Umoja wa Mataifa unatambua ni kwa kiasi gani habari potofu na habari za uongo kuwa ni mojawapo ya vikwazo vikuu vinavyokabili operesheni zake za kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Hii imesababisha Umoja huo kuhaha kila wakati kuona ni kwa vipi itakabiliana na habari hizo, iwe ni kupitia mafunzo kwa wanahabari, au kusaidia ujenzi wa vyombo vya habari, na hata kuzungumza na wananchi. Hivi karibuni Umoja Wa Mataifa kupitia Idara yake ya Ulinzi wa Amani, kitengo cha uadilifu wa habari, ulituma Tume yake Mashariki mwa DRC kukutana na wakazi ili kujua ni nini Umoja wa Mataifa unapaswa kufanya ili kupambana na habari potofu na za uongo nchini humo. Mwandishi wetu wa Mashariki mwa DRC, hususan jimboni Kivu Kaskazini, George Musubao alishuhudia ziara hiyo na ametuletea makala hii.
Duration:00:04:30
Patricia Kombo COP29: Ufadhili wa fedha utakuwa jawabu mujarabu kudhibiti mabadiliko ya tabianchi Afrika
11/13/2024
Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP29 leo ukiingia siku ya nne mjini Baku Azerbaijan vijana kutoka Afrika wataka ufadhili uongezwe kutoka mataifa makubwa hususan yanayochangia zaidi hewa ukaa ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi kwa mataifa yanayoendelea ambapomiongoni mwa waathirika wakubwa ni vijana. Asante Bosco na mmoja wa washiriki hao ni Patricial Kombo Mumbua kutoka Kenya akiwasilisha matakwa ya vijana katika mkutano huo, na akizungumza na UN News kuhusu ujumbe wake kwa COP29 amesema“Kwangu kama kiongozi wa vijana jambo la kwanza ni kuweza kupata zile fedha au kuzikusanya ili ziweze kusaidia mataifa ambayo yanapambana na kukabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi . Pili ni kuhakikisha kuwa viongozi kutoka mataifa ambayo yanazalisha zaidi hewa ukaa yanawajibika ili kuyafanya matifa ambayo yanaendelea kuweza kujilinda , kunufaika , kujiinua dhidi ya janga hilo na pia kujenga mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika jamii zao.”Na nini anachokitarajia katika mkutano huo wa COP29?“Ni kuweza kuona kuwa hili kongamano litaweza kuhamasisha upatikanaji wa hizo hela kwa mataifa ambayo yanakabiliwa na hizi changamoto za mabadiliko ya tabianchi, Na pia wakati ambapo mataifa yanaendelea kurekebisha michango yao ya kitaifa ya mabadiliko ya tabianchi au NDCs, waweze kuleta michango ambayo inaaambatana na zile changamoto ambazo mataifa yao yanazidi kuathiirika nazo za mabadiliko ya tabianchi.”Mbali ya masuala ya ufadhil mada zingine zinazotamalaki kwenye mijadala ya leo COP29 ni masuala ya nishani safi , mifumo ya tahadhari za mapemba na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa matifa ya visiwa vidogo vinavyoendelea.
Duration:00:01:51
13 NOVEMBA 2024
11/13/2024
Hii leo jaridani tunaangazi ufadhili kwa wakulima huku mkutano wa COP29 ukiendelea Baku, na madhara ya mafuriko kwa wakulima nchini Sudana Kusini tukimulika jinsi Umoja wa Mataifa wanavyohaha kuwasaidia. Makala inatupeleka nchini DRC na mashinani tunasalia huko huko Sudan Kusini, kulikoni?Kuongeza kiwango cha fedha kwenye ufadhili wa miradi ya kukabili na kuhimili tabianchi nchi ikiwa ni moja ya masuala muhimu yanayojadiliwa katika mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP29 huko Baku, Azerbaijan, leo ikiwa ni siku ya pili ya mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema bila kupunguza kwa kiasi kikubwa hewa chafuzi, na kuimarisha miradi ya kuhimili na kukabili mabadiliko ya tabianchi, kila uchumi duniani utakumbwa na madhara makubwa.Huko Maban, jimboni Upper Nile, kaskazini mashariki mwa Sudan Kusini, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linajenga vifaa vya kuhifadhi maji pamoja na makinga maji ili kuepusha mashamba dhidi ya mafuriko ya msimu yanayokumba eneo hilo mara kwa mara, eneo ambalo ardhi yake ina rutuba kwa ajili ya kilimo cha mazao ya chakula na biashara.Katika Makala George Musubao, mwandishi wetu huko Jimboni Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akimulika mkutano ulioandaliwa na watendaji wa Umoja wa Mataifa ya eneo hilo kuangalia jinsi ya kukabiliana na habari potofu na za uongo.Na mashinani tutakuwa Sudan Kusini, ambako shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP linasaidia jamii zilizoathiriwa na mafuriko kupata suluhisho la kudumu.Mwenyeji wako ni Bosco Cosmas, karibu!
Duration:00:10:00